Zab. 105:2-20 Swahili Union Version (SUV)

2. Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,Zitafakarini ajabu zake zote.

3. Jisifuni kwa jina lake takatifu,Na ufurahi moyo wao wamtafutao BWANA.

4. Mtakeni BWANA na nguvu zake,Utafuteni uso wake sikuzote.

5. Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya,Miujiza yake na hukumu za kinywa chake.

6. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake;Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.

7. Yeye, BWANA, ndiye Mungu wetu;Duniani mwote mna hukumu zake.

8. Analikumbuka agano lake milele;Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.

9. Agano alilofanya na Ibrahimu,Na uapo wake kwa Isaka.

10. Alilomthibitishia Yakobo liwe amri,Na Israeli liwe agano la milele.

11. Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani,Iwe urithi wenu mliopimiwa.

12. Walipokuwa watu wawezao kuhesabiwa,Naam, watu wachache na wageni ndani yake,

13. Wakatanga-tanga toka taifa hata taifa,Toka ufalme mmoja hata kwa watu wengine.

14. Hakumwacha mtu awaonee,Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao.

15. Akisema, Msiwaguse masihi wangu,Wala msiwadhuru nabii zangu.

16. Akaiita njaa iijilie nchi,Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.

17. Alimpeleka mtu mbele yao,Yusufu aliuzwa utumwani.

18. Walimwumiza miguu yake kwa pingu,Akatiwa katika minyororo ya chuma.

19. Hata wakati wa kuwadia neno lake,Ahadi ya BWANA ilimjaribu.

20. Mfalme alituma watu akamfungua,Mkuu wa watu akamwachia.

Zab. 105