Yos. 9:14-23 Swahili Union Version (SUV)

14. Basi hao watu wakatwaa katika vyakula vyao, wala wasitake shauri kinywani mwa BWANA.

15. Naye Yoshua akafanya amani pamoja nao, na kufanya agano nao, ili kwamba waachwe hai; na wakuu wa mkutano wakawaapia.

16. Kisha ikawa, mwisho wa siku ya tatu baada ya kufanya hilo agano nao, walisikia habari ya kuwa watu hao ni jirani zao, na ya kwamba waliketi kati yao.

17. Kisha wana wa Israeli walisafiri, wakaifikilia miji ya watu hao siku ya tatu. Basi miji ya watu hao ilikuwa ni hii, Gibeoni, na Kefira, na Beerothi, na Kiriath-yearimu.

18. Wana wa Israeli hawakuwapiga, kwa sababu wakuu wa mkutano walikuwa wamekwisha kuwaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli. Nao mkutano wote wakawanung’unikia hao wakuu.

19. Lakini wakuu wote waliwaambia mkutano wote, Sisi tumewaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli; basi sasa hatuwezi kuwagusa watu hawa.

20. Tutawafanyia neno hili, kisha tutawaacha wawe hai; hasira isije juu yetu, kwa ajili ya hicho kiapo tulichowaapia.

21. Wakuu waliwaambia, Waacheni wawe hai; basi wakawa wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya mkutano wote; vile vile kama hao wakuu walivyowaambia.

22. Basi Yoshua akawaita, akanena nao, na kuwaambia, Mbona ninyi mmetudanganya, huku mkisema, Sisi tu mbali sana na ninyi; nanyi kumbe! Mwakaa kati yetu?

23. Basi sasa mmelaaniwa kisha hatakosekana kuwapo mtu wa kwenu aliye mtumwa, wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.

Yos. 9