1. Kisha ikawa hapo wafalme wote waliokaa ng’ambo ya pili ya Yordani, hapo penye nchi ya vilima, na katika Shefela, na katika upande wa pwani yote ya bahari kubwa kuikabili Lebanoni, yaani, huyo Mhiti, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, waliposikia habari ya mambo hayo;
2. ndipo walipojikutanisha pamoja wenyewe kwa wenyewe, ili kupigana na Yoshua, na hao Israeli, kwa nia moja.
3. Lakini wenyeji wa Gibeoni waliposikia habari ya hayo yote Yoshua aliyokuwa amewatenda watu wa Yeriko, na wa Ai,
4. wao wakatenda kwa hila, nao wakaenda na kujifanya kama ndio wajumbe, wakaenda na magunia makuukuu juu ya punda zao, na viriba vya mvinyo vilivyokuwa vikuukuu vilivyoraruka-raruka, na kutiwa viraka;
5. na viatu vilivyotoboka na kushonwa-shonwa katika miguu yao, na mavao makuukuu waliyokuwa wanavaa; tena mkate wote wa chakula chao ulikuwa umekauka na kuingia koga.
6. Nao wakamwendea Yoshua hata maragoni huko Gilgali, nao wakamwambia yeye na watu wa Israeli, Sisi tumetoka nchi ya mbali sana; basi kwa hiyo fanyeni agano pamoja nasi.