Yos. 8:9-18 Swahili Union Version (SUV)

9. Basi Yoshua akawatuma; nao wakaenda hata hapo watakapootea, wakakaa kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa Ai; lakini Yoshua akalala usiku huo kati ya watu.

10. Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawakutanisha watu, kisha akatangulia kukwea kwenda Ai mbele ya hao watu, yeye na wazee wa Israeli.

11. Watu wote, hao wa vita, waliokuwa pamoja naye, wakaenda wakakaribia, na kufikilia mbele ya mji, wakatua upande wa kaskazini wa Ai; napo palikuwa na bonde kati ya yeye na Ai.

12. Kisha akatwaa watu kama elfu tano, akawaweka kuotea kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa huo mji.

13. Basi wakawaweka hao watu, jeshi zima lililokuwa upande wa kaskazini wa mji, na wale waliokuwa waotea upande wa magharibi wa mji; naye Yoshua akaenda usiku huo katikati ya hilo bonde.

14. Kisha ikawa hapo huyo mfalme wa Ai alipoona jambo hilo, ndipo walipofanya haraka, na wakaamka asubuhi na mapema, na watu waume wa mji wakatoka nje waende kupigana na Israeli, yeye na watu wake wote, kwa wakati ulioamriwa, kuikabili Araba; lakini hakujua ya kwamba walikuwako waviziao kinyume chake kwa upande wa nyuma wa mji.

15. Kisha Yoshua na watu wa Israeli wote walifanya kana kwamba wameshindwa mbele yao, wakakimbia kwa njia ya nyika.

16. Watu wote waliokuwa ndani ya mji waliitwa wakusanyike pamoja ili kuwafuatia; nao wakamfuatia Yoshua, wakasongea mbele na kuuacha mji.

17. Hakusalia mtu ye yote ndani ya Ai, au katika Betheli, asiyetoka nje kuwafuatia Israeli; wakauacha mji wazi na kuwafuatia Israeli.

18. Kisha BWANA akamwambia Yoshua, Haya, unyoshe huo mkuki ulio nao mkononi mwako, uuelekeze upande wa Ai; kwa kuwa nitautia mkononi mwako. Basi Yoshua akaunyosha huo mkuki uliokuwa mkononi mwake kuuelekea huo mji.

Yos. 8