24. Kisha ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamekwisha kuwaua wenyeji wote wa Ai katika bara, hapo katika nyika walipokuwamo wakiwafuatia, nao walikuwa wamekwisha anguka wote kwa makali ya upanga, hata walipokuwa wameangamizwa wote, ndipo Israeli wakarejea Ai, na kuupiga huo mji kwa makali ya upanga.
25. Wote walioanguka siku hiyo waume kwa wake, walikuwa ni kumi na mbili elfu, yaani, watu wote wa mji wa Ai.
26. Kwani huyo Yoshua hakuuzuia mkono wake, huo ulionyosha huo mkuki, hata hapo alipokuwa amewaangamiza kabisa wenyeji wote wa Ai.
27. Isipokuwa wanyama wa mji na nyara za mji Israeli wakatwaa wenyewe kuwa ni mapato yao, sawasawa na hilo neno la BWANA alilomwamuru Yoshua.
28. Basi Yoshua akaupiga moto mji wa Ai, na kuufanya kuwa ni chungu ya magofu hata milele, kuwa ni ukiwa hata siku hii ya leo.
29. Na huyo mfalme wa Ai akamtundika katika mti hata wakati wa jioni; kisha hapo jua lilipokuchwa Yoshua akaagiza, nao wakauondoa mzoga wake katika huo mti, na kuutupa hapo penye maingilio ya lango la mji, kisha wakaweka pale juu yake chungu kubwa ya mawe, hata hivi leo.
30. Ndipo Yoshua alijenga madhabahu kwa BWANA, Mungu wa Israeli katika mlima Ebali.