17. Hakusalia mtu ye yote ndani ya Ai, au katika Betheli, asiyetoka nje kuwafuatia Israeli; wakauacha mji wazi na kuwafuatia Israeli.
18. Kisha BWANA akamwambia Yoshua, Haya, unyoshe huo mkuki ulio nao mkononi mwako, uuelekeze upande wa Ai; kwa kuwa nitautia mkononi mwako. Basi Yoshua akaunyosha huo mkuki uliokuwa mkononi mwake kuuelekea huo mji.
19. Wale watu waliovizia wakainuka kwa upesi kutoka mahali pao, nao wakapiga mbio mara hapo alipokuwa amekwisha unyosha mkono wake, wakaingia ndani ya mji, na kuushika; nao wakafanya haraka kuuteketeza kwa moto huo mji.
20. Kisha hapo hao watu wa Ai walipotazama nyuma yao, wakaona, na tazama, moshi wa huo mji ulikuwa unapaa juu kwenda mawinguni, nao hawakuwa na nguvu za kukimbia huku wala huku; na wale watu waliokuwa wamekimbia kuenenda nyikani wakageuka na kuwarudia hao waliokuwa wakiwafuatia.
21. Basi hapo Yoshua na Israeli wote walipoona ya kwamba hao waliovizia wamekwisha kuushika huo mji, na ya kwamba moshi wa mji umepaa juu, ndipo wakageuka tena, na kuwaua watu wa Ai.
22. Tena hao; wengine wakatoka nje kuutoka huo mji kinyume chao; basi hivyo walikuwa wa katikati ya Israeli, wengine upande huu na wengine upande huu; nao wakawapiga, hata wasimwache hata mmoja miongoni mwao aliyesalia, wala kupona.
23. Kisha wakamshika mfalme wa Ai ali hai, nao wakamleta kwa Yoshua.
24. Kisha ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamekwisha kuwaua wenyeji wote wa Ai katika bara, hapo katika nyika walipokuwamo wakiwafuatia, nao walikuwa wamekwisha anguka wote kwa makali ya upanga, hata walipokuwa wameangamizwa wote, ndipo Israeli wakarejea Ai, na kuupiga huo mji kwa makali ya upanga.
25. Wote walioanguka siku hiyo waume kwa wake, walikuwa ni kumi na mbili elfu, yaani, watu wote wa mji wa Ai.
26. Kwani huyo Yoshua hakuuzuia mkono wake, huo ulionyosha huo mkuki, hata hapo alipokuwa amewaangamiza kabisa wenyeji wote wa Ai.
27. Isipokuwa wanyama wa mji na nyara za mji Israeli wakatwaa wenyewe kuwa ni mapato yao, sawasawa na hilo neno la BWANA alilomwamuru Yoshua.
28. Basi Yoshua akaupiga moto mji wa Ai, na kuufanya kuwa ni chungu ya magofu hata milele, kuwa ni ukiwa hata siku hii ya leo.
29. Na huyo mfalme wa Ai akamtundika katika mti hata wakati wa jioni; kisha hapo jua lilipokuchwa Yoshua akaagiza, nao wakauondoa mzoga wake katika huo mti, na kuutupa hapo penye maingilio ya lango la mji, kisha wakaweka pale juu yake chungu kubwa ya mawe, hata hivi leo.
30. Ndipo Yoshua alijenga madhabahu kwa BWANA, Mungu wa Israeli katika mlima Ebali.
31. Kama Musa, mtumishi wa BWANA, alivyowaamuru wana wa Israeli, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, madhabahu ya mawe yasiyochongwa, ambayo mtu hakutumia juu yake chombo cha chuma; nao wakatoa juu yake sadaka za kuteketezwa kwa BWANA, na kuchinja sadaka za amani.