Yos. 8:1-7 Swahili Union Version (SUV)

1. Kisha BWANA akamwambia Yoshua, Usiche, wala usifadhaike; wachukue watu wote wa vita waende pamoja nawe, nanyi inukeni, mwende Ai, angalia, mimi nimemtia mkononi mwako huyo mfalme wa Ai, na watu wake, na mji wake, na nchi yake;

2. nawe utautenda mji wa Ai na mfalme wake kama ulivyoutenda mji wa Yeriko na mfalme wake; lakini nyara zake na wanyama wake wa mji mtavitwaa kuwa mateka yenu wenyewe; huo mji uuwekee waoteaji upande wa nyuma.

3. Basi Yoshua akainuka, na watu wote wa vita pamoja naye, ili waende Ai; Yoshua akachagua watu thelathini elfu, watu mashujaa wenye uwezo, akawapeleka wakati wa usiku.

4. Akawaagiza, akasema, Angalieni, mtaotea kuuvizia ule mji, upande wa nyuma wa mji; msiende mbali sana na mji, lakini kaeni tayari nyote;

5. na mimi, na watu wote walio pamoja nami, tutaukaribia mji; kisha itakuwa, hapo watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo kwanza, sisi tutakimbia mbele yao;

6. nao watatoka nje watufuate, hata tuwavute waende mbali na mji wao; kwa kuwa watasema, Wakimbia mbele yetu, kama walivyofanya kwanza; nasi tutakimbia mbele yao;

7. basi ninyi mtainuka mtoke hapo mwoteapo, na kuushika mji; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, atautia mikononi mwenu.

Yos. 8