1. Kisha BWANA akamwambia Yoshua, Usiche, wala usifadhaike; wachukue watu wote wa vita waende pamoja nawe, nanyi inukeni, mwende Ai, angalia, mimi nimemtia mkononi mwako huyo mfalme wa Ai, na watu wake, na mji wake, na nchi yake;
2. nawe utautenda mji wa Ai na mfalme wake kama ulivyoutenda mji wa Yeriko na mfalme wake; lakini nyara zake na wanyama wake wa mji mtavitwaa kuwa mateka yenu wenyewe; huo mji uuwekee waoteaji upande wa nyuma.
3. Basi Yoshua akainuka, na watu wote wa vita pamoja naye, ili waende Ai; Yoshua akachagua watu thelathini elfu, watu mashujaa wenye uwezo, akawapeleka wakati wa usiku.
4. Akawaagiza, akasema, Angalieni, mtaotea kuuvizia ule mji, upande wa nyuma wa mji; msiende mbali sana na mji, lakini kaeni tayari nyote;