Yos. 7:20-26 Swahili Union Version (SUV)

20. Akani akamjibu Yoshua, akasema, Kweli nimefanya dhambi juu ya BWANA, Mungu wa Israeli, nami nimefanya mambo haya na haya.

21. Nilipoona katika nyara joho nzuri ya Babeli, na shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu, uzani wake shekeli hamsini, basi nalivitamani nikavitwaa; tazama, vimefichwa mchangani katikati ya hema yangu, na ile fedha chini yake.

22. Basi Yoshua akatuma wajumbe wakapiga mbio mpaka hemani; na tazama, vile vitu vilikuwa vimefichwa hemani mwake, na ile fedha chini yake.

23. Wakavitoa kutoka hapo katikati ya hema, wakavileta kwa Yoshua, na kwa wana wa Israeli wote, nao wakaviweka chini mbele za BWANA.

24. Kisha Yoshua, na Israeli wote pamoja naye, wakamtwaa Akani, mwana wa Zera, na ile fedha, na Lile joho, na ile kabari ya dhahabu, na wanawe, na binti zake, na ng’ombe zake, na punda zake, na kondoo zake, na hema yake, na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta juu hata bonde la Akori.

25. Yoshua akasema, Mbona umetufadhaisha hivi? BWANA atakufadhaisha wewe leo. Ndipo Israeli wote wakampiga kwa mawe, kisha wakawateketeza kwa moto, na kuwapiga kwa mawe.

26. Kisha wakakusanya juu yake chungu kubwa ya mawe hata leo; naye BWANA akauacha ukali wa hasira yake. Kwa sababu hiyo jina la mahali pale likaitwa, Bonde la Akori, hata hivi leo.

Yos. 7