14. Basi asubuhi mtaletwa karibu nami kabila kwa kabila; kisha itakuwa ya kwamba kabila ile atakayoitwaa BWANA itakaribia jamaa kwa jamaa; na jamaa ile atakayoitwaa BWANA itakaribia nyumba kwa nyumba; na nyumba ile atakayoitwaa BWANA itakaribia mtu kwa mtu.
15. Tena itakuwa ya kwamba yeye atakayetwaliwa, naye anacho kitu kile kilichowekwa wakfu, atateketezwa kwa moto, yeye na vitu vyote alivyo navyo; kwa sababu amelivunja agano la BWANA, na kwa sababu ametenda upumbavu katika Israeli.
16. Basi Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, akawasogeza Israeli kabila kwa kabila; kabila ya Yuda ikatwaliwa.
17. Akazisogeza jamaa za Yuda, akaitwaa jamaa ya Wazera; akaisogeza jamaa ya Wazera mtu kwa mtu; Zabdi akatwaliwa.
18. Akawasogeza watu wa nyumba yake mmoja mmoja; na Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila ya Yuda akatwaliwa.
19. Yoshua akamwambia Akani, Mwanangu, nakusihi, umtukuze BWANA, Mungu wa Israeli, ukaungame kwake; uniambie sasa ulilolitenda; usinifiche.
20. Akani akamjibu Yoshua, akasema, Kweli nimefanya dhambi juu ya BWANA, Mungu wa Israeli, nami nimefanya mambo haya na haya.