Yos. 7:12-16 Swahili Union Version (SUV)

12. Ndiposa wana wa Israeli hawawezi kusimama mbele ya adui zao; wakawapa visogo adui zao, kwa sababu wamelaaniwa; mimi sitakuwa pamoja nanyi tena, msipokiharibu kitu kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu.

13. Haya! Inuka, uwatakase watu, ukaseme, Jitakaseni, mwe tayari kesho; maana BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Kitu kilichowekwa wakfu kiko katikati yako, Ee Israeli; huwezi kusimama mbele ya adui zako, hata mtakapokiondoa kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu.

14. Basi asubuhi mtaletwa karibu nami kabila kwa kabila; kisha itakuwa ya kwamba kabila ile atakayoitwaa BWANA itakaribia jamaa kwa jamaa; na jamaa ile atakayoitwaa BWANA itakaribia nyumba kwa nyumba; na nyumba ile atakayoitwaa BWANA itakaribia mtu kwa mtu.

15. Tena itakuwa ya kwamba yeye atakayetwaliwa, naye anacho kitu kile kilichowekwa wakfu, atateketezwa kwa moto, yeye na vitu vyote alivyo navyo; kwa sababu amelivunja agano la BWANA, na kwa sababu ametenda upumbavu katika Israeli.

16. Basi Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, akawasogeza Israeli kabila kwa kabila; kabila ya Yuda ikatwaliwa.

Yos. 7