1. Lakini wana wa Israeli walifanya dhambi katika kitu kilichowekwa wakfu; maana Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila ya Yuda, alitwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; hasira ya BWANA ikawaka juu ya wana wa Israeli.
2. Kisha Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko mpaka mji wa Ai, ulio karibu na Bethaveni, upande wa mashariki wa Betheli, akawaambia, akisema, Pandeni juu mkaipeleleze nchi, basi wakapanda juu wakaupeleleza Ai.
3. Wakarejea kwa Yoshua wakamwambia, Wasiende watu wote, ila waende watu kama elfu mbili, tatu, wakaupige Ai; usiwataabishe watu wote kwa kuwaendesha huko; maana watu hao ni wachache tu.
4. Basi watu wakaenda huko wapata elfu tatu tu; nao wakakimbia mbele ya watu wa Ai.
5. Watu wa Ai wakawapiga watu kama thelathini na sita; wakawafuatia kutoka mbele ya mlango mpaka Shebarimu, wakawapiga huko kwenye matelemko; mioyo ya watu ikayeyuka, ikawa kama maji.
6. Yoshua akararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya sanduku la BWANA hata jioni, yeye na wazee wa Israeli; wakatia mavumbi vichwani mwao.
7. Yoshua akasema, Ee Bwana MUNGU, kwa nini umewavusha watu hawa mto wa Yordani, ili kututia katika mikono ya Waamori, na kutuangamiza? Laiti tungelikuwa radhi kukaa ng’ambo ya Yordani
8. Ee Bwana, niseme nini baada ya Israeli kuwapa visogo adui zao?
9. Maana Wakanaani na wenyeji wote wa nchi hii watasikia habari hii, nao watatuzingira, na kulifuta jina letu katika nchi. Nawe utafanya nini kwa ajili ya jina lako kuu?
10. BWANA akamwambia Yoshua, Haya! Inuka, mbona umeanguka kifudifudi hivi?
11. Israeli wamefanya dhambi, naam, wamelivunja agano langu nililowaagiza; naam, wametwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; tena wameiba, tena wameficha na kuvitia pamoja na vitu vyao wenyewe.