Yos. 5:1-8 Swahili Union Version (SUV)

1. Ikawa, wafalme wa Waamori, waliokaa ng’ambo ya Yordani pande za magharibi, na wafalme wote wa Wakanaani, waliokuwa karibu na bahari, waliposikia jinsi BWANA alivyoyakausha maji ya Yordani mbele ya wana wa Israeli, hata tulipokwisha kuvuka, basi mioyo yao iliyeyuka, wala haikuwamo roho ya nguvu ndani yao tena; kwa ajili ya wana wa Israeli.

2. Wakati huo BWANA akamwambia Yoshua, Haya, jifanyie visu vya mawe ya gumegume, watahiri tena wana wa Israeli mara ya pili.

3. Basi Yoshua akajifanyia visu vya mawe ya gumegume, akawatahiri wana wa Israeli huko Gibea-haaralothi.

4. Na sababu ya Yoshua kutahiri ni hii; watu wote waliotoka Misri, waliokuwa waume, hao watu waume wote waendao vitani walikufa katika bara njiani, baada ya wao kutoka Misri.

5. Kwa kuwa watu wote waliotoka walikuwa wamekwisha kutahiriwa; lakini watu wote waliozaliwa katika bara njiani walipokwisha kutoka Misri, hao hawakutahiriwa.

6. Kwa kuwa wana wa Israeli walitembea muda wa miaka arobaini barani, hata hilo taifa zima, yaani, watu waume waendao vitani, waliotoka Misri, walipokuwa wameangamia; kwa sababu hawakuisikiza sauti ya BWANA; nao ndio BWANA aliowaapia ya kwamba hatawaacha waione hiyo nchi, ambayo BWANA aliwaapia baba zao kwamba atatupa sisi; nchi ijaayo maziwa na asali.

7. Na watoto wao, aliowainua badala yao ndio hao aliowatahiri Yoshua; kwa kuwa wao walikuwa hawakutahiriwa, kwa maana walikuwa hawakuwatahiri njiani.

8. Ilikuwa walipokwisha kutahiriwa taifa zima, wakakaa kila mtu mahali pake maragoni, hata walipopoa.

Yos. 5