5. naye Yoshua akawaambia, Haya, piteni ninyi mtangulie mbele ya sanduku la BWANA, Mungu wenu, mwende pale katikati ya Yordani, mkatwae kila mtu wenu jiwe moja begani mwake, kwa kadiri ya hesabu ya kabila za wana wa Israeli;
6. ili kwamba jambo hili liwe ishara kati yenu, hapo watoto wenu watakapowauliza ninyi katika siku zijazo, wakisema, Ni nini maana yake mawe haya?
7. Ndipo mtakapowaambia, Ni kwa sababu maji ya Yordani yalitindika mbele ya sanduku la agano la BWANA; hapo lilipovuka Yordani, hayo maji ya Yordani yalitindika; na mawe haya yatakuwa ni ukumbusho kwa wana wa Israeli milele.
8. Basi wana wa Israeli walifanya vile vile kama Yoshua alivyowaamuru, nao wakatwaa mawe kumi na mawili pale katikati ya Yordani, kama BWANA alivyomwambia Yoshua, sawasawa na hesabu ya kabila za wana wa Israeli; wakayachukua wakavuka nayo hata mahali pale walipolala, nao wakayaweka nchi kuko huko.
9. Kisha Yoshua akapanga mawe kumi na mawili katikati ya Yordani, mahali pale miguu ya hao makuhani waliolichukua hilo sanduku la agano iliposimama; nayo yapo pale pale hata hivi leo.
10. Kwa kuwa makuhani waliolichukua hilo sanduku walisimama katikati ya Yordani, hata mambo yote BWANA aliyomwamuru Yoshua awambie hao watu yakaisha, sawasawa na hayo yote Musa aliyokuwa amemwamuru Yoshua; kisha hao watu wakafanya haraka wakavuka.
11. Ikawa watu wote walipokuwa wamekwisha vuka kabisa, hilo sanduku la BWANA likavuka, na hao makuhani, mbele ya macho ya hao watu.
12. Na wana wa Reubeni, na wana wa Gadi na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wakavuka, hali ya kuvaa silaha mbele ya wana wa Israeli, kama Musa alivyowaambia;
13. walipata kama watu arobaini elfu hesabu yao, wenye kuvaa silaha tayari kwa vita, waliovuka mbele ya BWANA, waende vitani, hata nchi tambarare za Yeriko.