13. walipata kama watu arobaini elfu hesabu yao, wenye kuvaa silaha tayari kwa vita, waliovuka mbele ya BWANA, waende vitani, hata nchi tambarare za Yeriko.
14. Siku ile BWANA alimtukuza Yoshua mbele ya macho ya Israeli wote; nao wakamcha, kama walivyokuwa wakimcha Musa, siku zote za maisha yake.
15. Kisha BWANA akanena na Yoshua, akamwambia,
16. Haya, uwaamuru makuhani, hao waliolichukua sanduku la ushuhuda, kwamba wakwee juu kutoka mle katika Yordani.
17. Basi Yoshua akawaamuru hao makuhani, akawaambia, Haya, kweeni mtoke Yordani.
18. Ilikuwa, hapo hao makuhani waliolichukua sanduku la agano la BWANA walipokwea juu kutoka mle kati ya Yordani, na nyayo za miguu yao hao makuhani zilipoinuliwa na kutiwa katika nchi kavu, ndipo maji ya Yordani yaliporudi mahali pake, na kujaa na kuipita mipaka yake, kama yalivyokuwa hapo kwanza.
19. Na hao watu wakakwea kutoka Yordani siku ya kumi ya mwezi wa kwanza, wakapiga kambi Gilgali, katika mpaka wa mashariki wa Yeriko.
20. Na yale mawe kumi na mawili waliyoyatwaa katikati ya Yordani Yoshua akayasimamisha Gilgali.
21. Akawaambia wana wa Israeli, akasema, Watoto wenu watakapowauliza baba zao katika siku zijazo, wakisema, Mawe haya maana yake ni nini?
22. Ndipo mtakapowaarifu watoto wenu mkisema, Israeli walivuka mto huu wa Yordani, kwa njia ya nchi kavu.
23. Kwa sababu BWANA, Mungu wenu aliyakausha maji ya Yordani, mbele yenu, hata mlipokwisha kuvuka kama BWANA, Mungu wenu, alivyoitenda Bahari ya Shamu, aliyoikausha mbele yetu hata tulipokwisha kuvuka;
24. watu wote wa duniani wapate kujua mkono wa BWANA, ya kuwa ni mkono wenye uweza, ili wamche BWANA, Mungu wenu, milele.