1. Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao wakatoka Shitimu, wakafika mto wa Yordani, yeye na wana wa Israeli wote, wakakaa hapo kabla ya kuvuka.
2. Ikawa baada ya siku tatu, maakida wakapita katikati ya marago,
3. wakawaamuru watu wote wakisema, Mtakapoliona sanduku la agano la BWANA, Mungu wenu, na makuhani Walawi wakilichukua, ndipo mtakapoondoka hapa mlipo na kulifuata.
4. Lakini, na iwe nafasi kati ya ninyi na lile sanduku, kama dhiraa elfu mbili kiasi chake; msilikaribie mpate kuijua njia ambayo hamna budi kuiendea; kwa maana hamjapita njia hii bado.
5. Yoshua akawaambia watu, Jitakaseni; maana kesho BWANA atatenda mambo ya ajabu kati yenu.
6. Kisha Yoshua akawaambia makuhani, akasema, Liinueni sanduku la agano, mkavuke mbele ya hao watu. Wakaliinua sanduku la agano, wakatangulia mbele ya watu.