4. Kisha nikampa huyo Isaka, Yakobo na Esau; nami nikampa Esau mlima Seiri aumiliki; Yakobo na watoto wake wakashuka Misri.
5. Kisha nikawatuma Musa na Haruni nikaipiga nchi ya Misri, kwa hayo yote niliyoyatenda kati yake; hatimaye nikawatoa ninyi.
6. Nikawatoa baba zenu watoke Misri; nanyi mkaifikilia bahari; Wamisri wakawafuatia baba zenu kwa magari na wapanda farasi mpaka bahari ya Shamu.
7. Nao walipomlilia BWANA, akaweka giza kati ya ninyi na Wamisri, akaileta bahari juu yao, akawafunikiza; nayo macho yenu yaliyaona mambo niliyoyatenda huko Misri; kisha mkakaa jangwani siku nyingi.
8. Kisha nikawaleta na kuwaingiza katika nchi ya Waamori waliokaa ng’ambo ya pili ya Yordani; nao wakapigana nanyi; nikawatia mikononi mwenu, mkaimiliki nchi yao; nami nikawaangamiza mbele yenu.
9. Ndipo Balaki, mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, akainuka, akapigana na Israeli; tena akatuma watu akamwita Balaamu, mwana wa Beori, aje awalaani;
10. lakini sikukubali kumsikiliza Balaamu; kwa hiyo akafuliza kuwabarikia ninyi; basi nikawatoa katika mkono wake.
11. Nanyi mliuvuka Yordani, mkafika Yeriko; nao watu wa Yeriko wakapigana nanyi, Mwamori, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhiti, na Mgirgashi, na Mhivi, na Myebusi; nami nikawatia mikononi mwenu.
12. Nikatuma mavu mbele yenu, waliowafukuza mbele yenu hao wafalme wawili wa Waamori, si kwa upanga wako, wala kwa upinde wako.
13. Nami nimewapa ninyi nchi msiyoitendea kazi, na miji msiyoijenga, nanyi mmekaa humo; mnakula matunda ya mashamba ya mizabibu na mizeituni msiyoipanda.
14. Basi sasa mcheni BWANA, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye BWANA.
15. Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA.
16. Hao watu wakajibu wakasema, Hasha! Tusimwache BWANA, ili kuitumikia miungu mingine;
17. kwa maana BWANA, Mungu wetu, yeye ndiye aliyetupandisha sisi na baba zetu kutoka nchi ya Misri; kutoka nyumba ya utumwa; naye ndiye aliyezifanya ishara zile kubwa mbele ya macho yetu, na kutulinda katika njia ile yote tuliyoiendea, na kati ya watu wa mataifa yote tuliopita katikati yao.
18. BWANA ndiye aliyewafukuza watu wa mataifa yote watoke mbele yetu, naam, Waamori waliokaa katika nchi hii; basi, kwa sababu hiyo sisi nasi tutamtumikia BWANA, maana yeye ndiye Mungu wetu.