10. lakini sikukubali kumsikiliza Balaamu; kwa hiyo akafuliza kuwabarikia ninyi; basi nikawatoa katika mkono wake.
11. Nanyi mliuvuka Yordani, mkafika Yeriko; nao watu wa Yeriko wakapigana nanyi, Mwamori, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhiti, na Mgirgashi, na Mhivi, na Myebusi; nami nikawatia mikononi mwenu.
12. Nikatuma mavu mbele yenu, waliowafukuza mbele yenu hao wafalme wawili wa Waamori, si kwa upanga wako, wala kwa upinde wako.
13. Nami nimewapa ninyi nchi msiyoitendea kazi, na miji msiyoijenga, nanyi mmekaa humo; mnakula matunda ya mashamba ya mizabibu na mizeituni msiyoipanda.
14. Basi sasa mcheni BWANA, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye BWANA.
15. Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA.
16. Hao watu wakajibu wakasema, Hasha! Tusimwache BWANA, ili kuitumikia miungu mingine;
17. kwa maana BWANA, Mungu wetu, yeye ndiye aliyetupandisha sisi na baba zetu kutoka nchi ya Misri; kutoka nyumba ya utumwa; naye ndiye aliyezifanya ishara zile kubwa mbele ya macho yetu, na kutulinda katika njia ile yote tuliyoiendea, na kati ya watu wa mataifa yote tuliopita katikati yao.
18. BWANA ndiye aliyewafukuza watu wa mataifa yote watoke mbele yetu, naam, Waamori waliokaa katika nchi hii; basi, kwa sababu hiyo sisi nasi tutamtumikia BWANA, maana yeye ndiye Mungu wetu.
19. Yoshua akawaambia watu, Hamwezi kumtumikia BWANA; kwa kuwa yeye ni Mungu mtakatifu; yeye ni Mungu mwenye wivu; hatawasamehe makosa yenu, wala dhambi zenu.
20. Kama mkimwacha BWANA na kuitumikia miungu migeni, ndipo atageuka na kuwatenda mabaya na kuwaangamiza, baada ya kuwatendea mema.
21. Lakini hao watu wakamwambia Yoshua, La! Lakini tutamtumikia BWANA.
22. Yoshua akawaambia watu, Ninyi mmekuwa mashahidi juu ya nafsi zenu, ya kuwa mmemchagua BWANA, ili kumtumikia yeye. Wakasema, Sisi tu mashahidi.
23. Akasema, Basi sasa, iondoeni miungu migeni iliyo kati yenu, mkaielekeze mioyo yenu kwa BWANA, Mungu wa Israeli.
24. Ndipo hao watu wakamwambia Yoshua, BWANA, Mungu wetu, ndiye tutakayemtumikia; na sauti yake ndiyo tutakayoitii.
25. Basi Yoshua akafanya agano na wale watu siku ile, akawapa amri na agizo huko Shekemu.
26. Yoshua akayaandika maneno haya katika kitabu cha torati ya Mungu; kisha akatwaa jiwe kubwa, akalisimamisha huko, chini ya ule mwaloni uliokuwa karibu na patakatifu pa BWANA.