1. Yoshua akawakusanya kabila zote za Israeli huko Shekemu, akawaita wazee wa Israeli, na wakuu wao, na waamuzi wao, na maakida wao nao wakahudhuria mbele za Mungu.
2. Yoshua akawaambia watu wote, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Baba zenu hapo zamani walikaa ng’ambo ya Mto, maana Tera, baba yake Ibrahimu, naye ni baba yake Nahori; wakaitumikia miungu mingine.
3. Nami nikamtwaa Ibrahimu baba yenu toka ng’ambo ya Mto, nikamwongoza katika nchi yote ya Kanaani; nikaongeza uzao wake, nikampa Isaka.
4. Kisha nikampa huyo Isaka, Yakobo na Esau; nami nikampa Esau mlima Seiri aumiliki; Yakobo na watoto wake wakashuka Misri.
5. Kisha nikawatuma Musa na Haruni nikaipiga nchi ya Misri, kwa hayo yote niliyoyatenda kati yake; hatimaye nikawatoa ninyi.
6. Nikawatoa baba zenu watoke Misri; nanyi mkaifikilia bahari; Wamisri wakawafuatia baba zenu kwa magari na wapanda farasi mpaka bahari ya Shamu.
7. Nao walipomlilia BWANA, akaweka giza kati ya ninyi na Wamisri, akaileta bahari juu yao, akawafunikiza; nayo macho yenu yaliyaona mambo niliyoyatenda huko Misri; kisha mkakaa jangwani siku nyingi.
8. Kisha nikawaleta na kuwaingiza katika nchi ya Waamori waliokaa ng’ambo ya pili ya Yordani; nao wakapigana nanyi; nikawatia mikononi mwenu, mkaimiliki nchi yao; nami nikawaangamiza mbele yenu.
9. Ndipo Balaki, mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, akainuka, akapigana na Israeli; tena akatuma watu akamwita Balaamu, mwana wa Beori, aje awalaani;