6. Basi Yoshua akawabarikia, na kuwapa ruhusa waende zao; nao wakaenda mahemani kwao.
7. Basi Musa alikuwa amewapa hiyo nusu moja ya kabila ya Manase urithi katika Bashani; lakini hiyo nusu ya pili Yoshua aliwapa urithi kati ya ndugu zao, ng’ambo ya Yordani upande wa kuelekea magharibi. Zaidi ya hayo Yoshua, hapo alipowapeleka waende zao mahemani kwao, akawabarikia,
8. kisha akanena nao, na kuwaambia, Rudini na mali mengi mahemani kwenu, na ng’ombe wengi sana, na fedha, na dhahabu, na shaba, na chuma, na mavao mengi sana; mzigawanye na ndugu zenu hizo nyara za adui zenu.
9. Basi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase wakarudi, wakatoka kwa wana wa Israeli katika Shilo, ulioko nchi ya Kanaani, ili waende nchi ya Gileadi, hiyo nchi ya milki yao, waliyokuwa wanaimiliki, sawasawa na amri ya BWANA kwa mkono wa Musa.
10. Nao walipofika pande za Yordani, zilizo katika nchi ya Kanaani, hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na nusu ya kabila ya Manase, wakajenga madhabahu huko karibu na Yordani, iliyoonekana kuwa ni madhabahu kubwa.
11. Wana wa Israeli walisikia ikinenwa, Tazama, wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wamejenga madhabahu huko upande wa mbele wa nchi ya Kanaani, katika nchi iliyo karibu na Yordani, kwa upande huo ulio milki ya wana wa Israeli.
12. Basi, wana wa Israeli waliposikia habari hiyo, mkutano wote wa wana wa Israeli wakakutanika pamoja huko Shilo, ili waende kupigana nao.
13. Kisha wana wa Israeli wakatuma wajumbe waende kwa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, hata nchi ya Gileadi; nao ni hawa, Finehasi mwana wa Eleazari kuhani;
14. na pamoja naye wakuu kumi, mkuu mmoja wa nyumba ya mababa kwa ajili ya kila kabila ya Israeli; nao kila mmoja alikuwa ni kichwa cha nyumba ya mababa katika maelfu ya Israeli.
15. Nao wakawafikilia hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, katika nchi ya Gileadi, na wakasema nao, wakinena,
16. Mkutano wote wa BWANA wanena, Ni kosa gani hili mlilolikosa juu ya Mungu wa Israeli, hata mkakengeuka hivi leo na kuacha kumwandama BWANA, katika kujijengea madhabahu, na kuasi hivi leo juu ya BWANA?
17. Je! Ule uovu wa Peori haututoshi, ambao hamjajitakasa nafsi zenu katika huo hata hivi leo, ijapokuwa ilikuja tauni juu ya mkutano wa BWANA,
18. hata ikawa hamna budi hivi leo kugeuka na kuacha kumwandama BWANA? Kisha itakuwa, kwa kuwa ninyi mwamwasi BWANA hivi leo, kwamba kesho yeye atakasirika na mkutano wote wa Israeli.