26. Kwa ajili ya hayo tulisema, Na tufanye tayari ili kujijengea madhabahu, si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, wala kwa sadaka yo yote;
27. bali itakuwa ni ushahidi kati ya sisi na ninyi, tena kati ya vizazi vyetu baada yetu, ili kwamba tufanye huo utumishi wa BWANA mbele yake kwa njia ya sadaka zetu za kuteketezwa, na kwa dhabihu zetu, na kwa sadaka zetu za amani; ili kwamba wana wenu wasiwaambie wana wetu katika zamani zijazo, Ninyi hamna fungu katika BWANA.
28. Kwa hiyo tulisema, Itakuwa, hapo watakapotuambia neno kama hilo, au kuwaambia watu wa vizazi vyetu katika zamani zijazo neno kama hilo, ndipo sisi tutawaambia, Angalieni huu mfano wa madhabahu ya BWANA, walioufanya baba zetu, si kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, wala kwa ajili ya dhabihu; lakini ni ushahidi kati ya sisi na ninyi.
29. Mungu na atuzuie msimwasi BWANA, na kukengeuka hivi leo na kuacha kumwandama BWANA, hata mkajenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, au sadaka za unga, au dhabihu, mbali na ile madhabahu ya BWANA, Mungu wetu, iliyo huko mbele ya maskani yake.