Yos. 2:1-16 Swahili Union Version (SUV)

1. Yoshua, mwana wa Nuni, akawatuma watu wawili kutoka Shitimu kwa siri, ili kupeleleza, akawaambia, Enendeni mkaitazame nchi hii, na Yeriko. Wakaenda wakafika nyumbani kwa kahaba mmoja jina lake aliitwa Rahabu, wakalala huko.

2. Mfalme wa Yeriko akaambiwa, kusema, Tazama, watu wawili wa wana wa Israeli wameingia humu leo usiku, ili kuipeleleza nchi.

3. Mfalme wa Yeriko akatuma watu kwa Rahabu, akasema, Watoe watu wale waliokuja kwako, walioingia ndani ya nyumba yako, maana wamekuja ili kuipeleleza nchi.

4. Yule mwanamke akawatwaa wale watu wawili, akawaficha, akasema, Naam, wale watu walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka;

5. ikawa kama wakati wa kufungwa lango la mji, kulipokuwa giza, watu wale wakatoka, wala sijui walikokwenda; wafuateni upesi, maana mtawapata.

6. Lakini yeye alikuwa amewapandisha darini, akawaficha kwa mabua ya kitani, aliyokuwa ameyatandika juu ya dari.

7. Basi hao watu wakawafuata kwa njia iendayo Yordani mpaka vivukoni; na mara wale watu waliowafuatia walipokwisha kutoka, wakalifunga lango.

8. Tena kabla hawajalala akawaendea juu darini,

9. akawaambia wale wanaume, Mimi najua ya kuwa BWANA amewapa ninyi nchi hii, na ya kuwa hofu imetuangukia mbele yenu, na ya kuwa wenyeji wote wa nchi wanayeyuka mbele yenu.

10. Maana tumesikia jinsi BWANA alivyoyakausha maji ya bahari ya Shamu mbele yenu, hapo mlipotoka Misri, tena mambo hayo mliyowatendea wafalme wawili wa Waamori waliokuwa huko ng’ambo ya Yordani, yaani, Sihoni na Ogu, mliowaangamiza kabisa.

11. Na mara tuliposikia hayo mioyo yetu iliyeyuka, wala haukusalia ujasiri wo wote katika mtu awaye yote, kwa sababu yenu; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu, katika mbingu juu na katika nchi chini.

12. Basi sasa, nawasihi, niapieni kwa BWANA, kwa kuwa nimewatendea ihisani, ya kwamba ninyi nanyi mtaitendea ihisani nyumba ya baba yangu; tena nipeni alama ya uaminifu;

13. ya kwamba mtawaponya hai baba yangu na mama yangu, na ndugu zangu wanaume na wanawake, na vitu vyote walivyo navyo, na kutuokoa roho zetu na kufa.

14. Wale wanaume wakamwambia, Uhai wetu badala ya uhai wenu, ikiwa hamwitangazi habari ya shughuli yetu hii; kisha itakuwa, wakati BWANA atakapotupa nchi hii, tutakutendea kwa ihisani na uaminifu.

15. Ndipo akawashusha kwa kamba dirishani, maana nyumba yake ilikuwa katika ukuta wa mji; naye alikaa ukutani.

16. Akawaambia, Enendeni zenu mlimani, wale wanaowafuatia wasije wakawapata; mkajifiche huko siku tatu hata wao wanaowafuatia watakaporudi; kisha enendeni zenu.

Yos. 2