1. Kisha hii ndiyo kura iliyoiangukia kabila ya Manase; maana, yeye alikuwa ni mzaliwa wa kwanza, wa Yusufu. Katika habari za Makiri, mzaliwa wa kwanza wa Manase, babaye Gileadi, kwa sababu alikuwa mtu wa vita, basi alikuwa na Gileadi na Bashani.
2. Na kura ilikuwa ni ya hao wana wa Manase waliosalia kwa kuandama jamaa zao; kwa wana wa Abiezeri, na kwa wana wa Heleki, na kwa wana wa Asrieli, na kwa wana wa Shekemu, na kwa wana wa Heferi, na kwa wana wa Shemida; hao ndio wana waume wa Manase, mwana wa Yusufu, kwa kuandama jamaa zao.
3. Lakini Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, hakuwa na wana waume ila binti; na majina ya hao binti zake walikuwa wakiitwa Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa.
4. Nao wakakaribia mbele ya Eleazari, kuhani, na mbele ya Yoshua, mwana wa Nuni, na mbele ya mashehe, wakasema, BWANA alimwamuru Musa kutupa sisi urithi kati ya ndugu zetu; basi kwa kuiandama hiyo amri ya BWANA akawapa urithi kati ya ndugu za baba yao.
5. Kisha kura zilizomwangukia Manase zilikuwa ni sehemu kumi, mbali na nchi ya Gileadi na Bashani, iliyo ng’ambo ya Yordani;
6. kwa sababu hao binti za Manase walikuwa na urithi katika wanawe waume; na nchi ya Gileadi ilikuwa ni mali ya hao wana waume wa Manase waliosalia.
7. Mpaka wa Manase ulikuwa kutoka Asheri hata Mikmeta, ulioelekea Shekemu; tena mpaka ukaendelea upande wa kuume, hata kuwafikilia wenyeji wa Entapua.
8. Hiyo nchi ya Tapua ilikuwa ni mali ya Manase; lakini ule mji wa Tapua uliokuwa katika mpaka wa Manase ulikuwa ni mali ya wana wa Efraimu.