8. kisha mpaka ukaendelea karibu na bonde la mwana wa Hinomu, na kufikilia ubavuni mwa huyu Myebusi upande wa kusini (ndio Yerusalemu); kisha mpaka ukaendelea hata kilele cha mlima ulio pale mkabala wa bonde la Hinomu upande wa magharibi, lililo pale mwisho wa bonde la Warefai upande wa kaskazini;
9. kisha mpaka ulipigwa kutoka juu ya mlima huo hata kufikilia chemchemi ya maji ya Neftoa kisha ukatokea hata miji ya kilima cha Efroni; kisha mpaka ulipigwa hata kufikilia Baala (ndio Kiriath-yearimu);
10. kisha mpaka ukazunguka kutoka Baala kwendelea upande wa magharibi hata kilima Seiri, kisha ukaendelea hata upande wa mlima wa Yearimu upande wa kaskazini (huo ndio Kesaloni), kisha ukatelemkia Beth-shemeshi, na kwendelea karibu na Timna;
11. kisha mpaka ukatokea hata kufikilia upande wa Ekroni upande wa kaskazini; tena mpaka ulipigwa hata Shikroni, na kwendelea hata kilima cha Baala, kisha ukatokea hapo Yabneeli; na matokeo ya mpaka yalikuwa baharini.
12. Na mpaka wa upande wa magharibi ulifikilia hata bahari kubwa, na mpaka wake. Huo ndio mpaka wa wana wa Yuda kwa kuzunguka kote kote sawasawa na jamaa zao.
13. Kisha alimpa huyo Kalebu mwana wa Yefune sehemu kati ya wana wa Yuda, kama BWANA alivyomwamuru Yoshua, maana ni Kiriath-arba, ni huyo Arba aliyekuwa babaye Anaki (huo ndio Hebroni).
14. Huyo Kalebu aliwafukuza watoke hapo hao wana watatu wa Anaki, nao ni Sheshai, na Ahimani, na Talmai, wana wa Anaki.
15. Kisha akakwea kutoka huko ili kuwaendea wenyeji wa Debiri; jina la Debiri hapo kwanza lilikuwa Kiriath-seferi.
16. Kalebu akasema, Yeye atakayeupiga Kiriath-seferi na kuutwaa, mimi nitampa Aksa binti yangu awe mkewe.
17. Naye Othnieli mwana wa Kenazi, nduguye Kalebu, aliutwaa; basi akampa Aksa binti yake awe mkewe.
18. Kisha ikawa, hapo huyo mwanamke alipokwenda kwa mumewe, akamtaka aombe shamba kwa baba yake; akashuka katika punda wake; Kalebu akamwuliza, Wataka nini?
19. Huyo mwanamke akasema, Nipe baraka; kwa kuwa umeniweka katika nchi ya kusini, unipe na chemchemi za maji pia. Ndipo akampa chemchemi za maji ya juu, na chemchemi za maji ya chini.
20. Huu ndio urithi wa kabila ya wana wa Yuda sawasawa na jamaa zao.