5. Vile vile kama BWANA alivyomwamuru Musa, hao wana wa Israeli walifanya vivyo, nao wakaigawanya hiyo nchi.
6. Wakati huo wana wa Yuda walimkaribia Yoshua hapo Gilgali; na Kalebu, mwana wa Yefune, huyo Mkenizi, akamwambia, Wewe wajua hilo neno BWANA alilomwambia Musa, huyo mtu wa Mungu, katika habari zangu, na katika habari zako wewe, tulipokuwa katika Kadesh-barnea.
7. Mimi nilikuwa mtu wa miaka arobaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa BWANA aliponituma niende kutoka Kadesh-barnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama ilivyokuwa ndani ya moyo wangu.
8. Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja nami waliiyeyusha mioyo ya watu; ila mimi nilimfuata BWANA, Mungu wangu, kwa utimilifu.
9. Kisha Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi ambayo miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele, kwa sababu wewe umemfuata BWANA, Mungu wako, kwa utimilifu.