1. Kisha hizi ndizo nchi ambazo wana wa Israeli walizitwaa katika nchi ya Kanaani, ambazo Eleazari kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni, na vichwa vya nyumba za mababa wa kabila za Israeli, waliwagawanyia,
2. kwa kuandama hiyo kura ya urithi wao, vile vile kama BWANA alivyoamuru kwa mkono wa Musa, kwa ajili ya hizo kabila kenda, na hiyo nusu ya kabila.
3. Kwa kuwa Musa alikuwa amekwisha kuwapa urithi hizo kabila mbili na nusu, ng’ambo ya pili ya Yordani; lakini hakuwapa Walawi urithi uwao wote kati yao.
4. Kwa kuwa wana wa Yusufu walikuwa kabila mbili, Manase na Efraimu; nao hawakuwapa Walawi sehemu katika hiyo nchi, isipokuwa waliwapa miji wapate kuikaa, pamoja na viunga vyake kwa ajili ya wanyama wao wa mifugo, na kwa ajili ya riziki zao.
5. Vile vile kama BWANA alivyomwamuru Musa, hao wana wa Israeli walifanya vivyo, nao wakaigawanya hiyo nchi.
6. Wakati huo wana wa Yuda walimkaribia Yoshua hapo Gilgali; na Kalebu, mwana wa Yefune, huyo Mkenizi, akamwambia, Wewe wajua hilo neno BWANA alilomwambia Musa, huyo mtu wa Mungu, katika habari zangu, na katika habari zako wewe, tulipokuwa katika Kadesh-barnea.