1. Basi Yoshua alipokuwa mzee, na kwendelea sana miaka yake, BWANA akamwambia, Wewe umekuwa mzee na kwendelea sana miaka yako, kisha inasalia nchi nyingi sana bado kumilikiwa.
2. Nchi iliyosalia ni hii; nchi zote za Wafilisti, na Wageshuri wote;
3. kutoka Shihori, hicho kijito kilichokabili Misri, hata mpaka wa Ekroni upande wa kaskazini, nchi inayohesabiwa kuwa ni ya hao Wakanaani; mashehe matano wa hao Wafilisti; Wagaza, na Waashdodi, na Waashkeloni, na Wagiti, na Waekroni; tena Waavi,
4. upande wa kusini; nchi yote ya Wakanaani na Meara iliyo ya Wasidoni, mpaka Afeka, hata mpaka wa Waamori;
5. na nchi ya Wagebali na Lebanoni yote, upande wa kuelekea maawio ya jua, kutoka Baal-gadi ulio chini ya mlima wa Hermoni mpaka kufikilia maingilio ya Hamathi;
6. na watu wote wenye kuikaa nchi ya vilima kutoka Lebanoni hata Misrefoth-maimu, maana, hao Wasidoni wote; hao wote nitawafukuza watoke mbele ya wana wa Israeli; lakini wewe uwape Israeli kuwa ni urithi wao, kama nilivyokuamuru.
7. Basi sasa gawanya nchi hii, iwe urithi wa hizi kabila kenda, na nusu ya kabila ya Manase.