14. Tena nyara zote za miji hiyo, na wanyama wa miji, wana wa Israeli walitwaa kuwa nyara zao wenyewe; lakini kila mtu wakampiga kwa makali ya upanga, hata walipokuwa wamewaangamiza wote, wala hawakumsaza mmoja mwenye kuvuta pumzi.
15. Vile vile kama BWANA alivyomwamuru Musa mtumishi wake, ndivyo Musa alivyomwamuru Yoshua; naye Yoshua akafanya vivyo; hakukosa kufanya neno lo lote katika hayo yote BWANA aliyomwamuru Musa.
16. Hivyo Yoshua akatwaa nchi hiyo yote, hiyo nchi ya vilima, na nchi yote ya Negebu, na nchi yote ya Gosheni, na hiyo Shefela, na hiyo Araba na nchi ya vilima vilima ya Israeli, na hiyo nchi tambarare;
17. tangu kilima cha Halaki, kiendeleacho upande wa Seiri, mpaka Baal-gadi katika bonde la Lebanoni chini ya kilima cha Hermoni; naye akawatwaa wafalme wao wote, akawapiga, na kuwaua.
18. Yoshua akapiga vita siku nyingi na wafalme hao wote.
19. Haukuwapo mji hata mmoja uliofanya amani na wana wa Israeli, isipokuwa ni wale Wahivi wenye kukaa Gibeoni; wakaitwaa yote vitani.
20. Kwa kuwa lilikuwa ni la BWANA kuifanya mioyo yao kuwa migumu, hata wakatoka kupigana na Israeli, ili apate kuwaangamiza kabisa, wasihurumiwe lakini apate kuwaangamiza, kama vile BWANA alivyomwamuru Musa.
21. Wakati huo Yoshua akaenda na kuwakatilia mbali hao Waanaki watoke nchi ya vilima, kutoka Hebroni, na kutoka Debiri, na kutoka Anabu, na kutoka katika nchi yote ya vilima vilima ya Yuda, na kutoka katika nchi yote ya vilima vilima ya Israeli; Yoshua akawaangamiza kabisa na miji yao.
22. Hawakusalia Waanaki hata mmoja katika nchi ya wana wa Israeli; isipokuwa katika Gaza, na katika Gathi, na katika Ashdodi walisalia.
23. Basi Yoshua akaitwaa hiyo nchi yote, sawasawa na hayo yote BWANA aliyokuwa amemwambia Musa; Yoshua naye akawapa Israeli kuwa ni urithi wao, sawasawa na walivyogawanyikana kwa kabila zao. Kisha nchi ikatulia isiwe na vita tena.