12. Tena miji yote ya wafalme hao, na wafalme wake wote, Yoshua akawatwaa, akawapiga kwa makali ya upanga, na kuwaangamiza kabisa; vile vile kama huyo Musa mtumishi wa BWANA alivyomwamuru.
13. Lakini katika habari ya miji hiyo iliyosimama katika vilima vyao, Israeli hawakuipiga moto miji hiyo, isipokuwa ni mji wa Hazori tu; mji huo Yoshua aliupiga moto.
14. Tena nyara zote za miji hiyo, na wanyama wa miji, wana wa Israeli walitwaa kuwa nyara zao wenyewe; lakini kila mtu wakampiga kwa makali ya upanga, hata walipokuwa wamewaangamiza wote, wala hawakumsaza mmoja mwenye kuvuta pumzi.
15. Vile vile kama BWANA alivyomwamuru Musa mtumishi wake, ndivyo Musa alivyomwamuru Yoshua; naye Yoshua akafanya vivyo; hakukosa kufanya neno lo lote katika hayo yote BWANA aliyomwamuru Musa.
16. Hivyo Yoshua akatwaa nchi hiyo yote, hiyo nchi ya vilima, na nchi yote ya Negebu, na nchi yote ya Gosheni, na hiyo Shefela, na hiyo Araba na nchi ya vilima vilima ya Israeli, na hiyo nchi tambarare;
17. tangu kilima cha Halaki, kiendeleacho upande wa Seiri, mpaka Baal-gadi katika bonde la Lebanoni chini ya kilima cha Hermoni; naye akawatwaa wafalme wao wote, akawapiga, na kuwaua.
18. Yoshua akapiga vita siku nyingi na wafalme hao wote.