Yos. 11:1-10 Swahili Union Version (SUV)

1. Kisha ikawa, hapo huyo Yabini, mfalme wa Hazori, aliposikia habari ya mambo hayo, akatuma mjumbe aende kwa Yobabu, mfalme wa Madoni, na kwa mfalme wa Shimroni, na mfalme wa Akshafu,

2. na hao wafalme waliokuwa upande wa kaskazini, katika nchi ya vilima, na katika Araba upande wa kusini wa Kinerethi, na katika Shefela, na katika nchi zilizoinuka za Dori upande wa magharibi,

3. na kwa Mkanaani upande wa mashariki, na upande wa magharibi, na kwa Mwamori, na Mhiti, na Mperizi na Myebusi katika nchi ya vilima, na kwa Mhivi pale chini ya Hermoni katika nchi ya Mispa.

4. Nao wakatoka nje, wao na jeshi zao zote pamoja nao, watu wengi mno, kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi, pamoja na farasi na magari mengi sana.

5. Wafalme hao wote wakakutana pamoja; wakaenda na kupanga mahema yao pamoja hapo penye maji ya Meromu, ili kupigana na Israeli.

6. BWANA akamwambia Yoshua, Usiche wewe kwa ajili ya hao; kwani kesho wakati kama huu nitawatoa hali wameuawa wote mbele ya Israeli; utawatema farasi zao, na magari yao utayapiga moto.

7. Basi Yoshua akaenda, na watu wote wa vita pamoja naye, ili kupigana nao hapo penye maji ya Meromu ghafula; wakawaangukia.

8. BWANA akawatia mkononi mwa Israeli, nao wakawapiga, na kuwafukuza hata kufikilia Sidoni ulio mkuu, na hata kufikilia Misrefoth-maimu, tena hata kufikilia bonde la Mispa upande wa mashariki; wakawapiga hata wasiwasaze hata mtu mmoja aliyesalia.

9. Yoshua akawafanyia vile vile kama BWANA alivyomwamuru; akawatema farasi zao, na magari yao akayapiga moto.

10. Yoshua akarudi wakati huo na kuutwaa Hazori, akampiga mfalme wa Hazori kwa upanga; kwa kuwa Hazori hapo kwanza ulikuwa ni kichwa cha falme hizo zote.

Yos. 11