Yos. 10:28-40 Swahili Union Version (SUV)

28. Siku hiyo Yoshua akautwaa mji wa Makeda, akaupiga kwa makali ya upanga, na mfalme wake; akawaangamiza kabisa na wote pia waliokuwamo ndani yake, hakumwacha hata mmoja aliyesalia; naye akamfanyia huyo mfalme wa Makeda kama alivyomfanyia huyo mfalme wa Yeriko.

29. Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Makeda, mpaka Libna, na Israeli wote pamoja naye, nao wakapiga Libna;

30. BWANA akautia na mji huo pia pamoja na mfalme wake mkononi mwa Israeli; naye akaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake; hakumwacha hata mmoja aliyesalia ndani yake; naye akamtenda mfalme wake kama alivyomtenda huyo mfalme wa Yeriko.

31. Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Libna, na Israeli wote pamoja naye, wakafika Lakishi, wakapanga marago mbele yake na kupigana nao;

32. BWANA akautia huo mji wa Lakishi mkononi mwa Israeli, naye akautwaa siku ya pili, akaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake, sawasawa na hayo yote aliyoutenda Libna.

33. Wakati huo Horamu, mfalme wa Gezeri, akakwea ili kuusaidia Lakishi, lakini Yoshua akampiga yeye na watu wake, hata asimsazie hata mtu mmoja.

34. Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Lakishi, na Israeli wote pamoja naye, hata wakafikilia Egloni; nao wakapanga marago mbele yake, na kupigana nao;

35. siku iyo hiyo wakautwaa, nao wakaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake akawaangamiza kabisa siku hiyo, sawasawa na hayo yote aliyoufanyia mji wa Lakishi.

36. Kisha Yoshua akakwea kutoka hapo Egloni, na Israeli wote pamoja naye, hata wakafikilia Hebroni; nao wakapigana nao;

37. wakautwaa, na kuupiga kwa makali ya upanga, na mfalme wake, na miji yake yote, na wote waliokuwamo ndani yake; hakumwacha aliyesalia hata mtu mmoja, sawasawa na hayo yote aliyoufanyia huo mji wa Egloni; lakini akauangamiza kabisa, na wote pia waliokuwamo ndani yake.

38. Kisha Yoshua akarudi, na Israeli wote pamoja naye, hata Debiri; nao wakapigana nao;

39. kisha akautwaa, na mfalme wake, na miji yake yote; nao wakawapiga kwa makali ya upanga, wakawaangamiza kabisa wote pia waliokuwamo ndani yake; hakumwacha hata mmoja aliyesalia; kama alivyoufanyia Hebroni aliufanyia na Debiri vivyo, na mfalme wake; kama alivyoufanyia Libna, na mfalme wake.

40. Basi Yoshua akaipiga nchi hiyo yote, nchi ya vilima, na nchi ya Negebu, na nchi ya Shefela, na nchi ya matelemko, na wafalme wake wote; hakumwacha aliyesalia hata mmoja; lakini akawaharibu kabisa wote waliokuwa wavuta pumzi, kama BWANA, Mungu wa Israeli, alivyoamuru.

Yos. 10