10. Yafueni majembe yenu yawe panga, na miundu yenu iwe mikuki; aliye dhaifu na aseme, Mimi ni hodari.
11. Fanyeni haraka, mje, enyi mataifa yote, wa pande zote, jikusanyeni pamoja; na huko watelemshe mashujaa wako wote, Ee BWANA.
12. Mataifa na wajihimize, wakapande juu katika bonde la Yehoshafau; maana huko ndiko nitakakoketi niwahukumu mataifa yote yaliyo pande zote.
13. Haya! Utieni mundu, maana mavuno yameiva; njoni, kanyageni; kwa maana shinikizo limejaa, mapipa nayo yanafurika; kwani uovu wao ni mwingi sana.
14. Makutano makubwa, makutano makubwa, wamo katika bonde la kukata maneno! Kwa maana siku ya BWANA i karibu, katika bonde la kukata maneno.
15. Jua na mwezi vimetiwa giza, na nyota zimeacha kuangaza.
16. Naye BWANA atanguruma toka Sayuni, atatoa sauti yake toka Yerusalemu; na mbingu na nchi zitatetemeka; lakini BWANA atakuwa kimbilio la watu wake, na ngome ya wana wa Israeli.
17. Hivyo ndivyo mtakavyojua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, nikaaye Sayuni, mlima wangu mtakatifu; ndipo Yerusalemu utakapokuwa mtakatifu, wala wageni hawatapita tena ndani yake kamwe.
18. Tena itakuwa siku ile, ya kwamba milima itadondoza divai tamu, na vilima vitatiririka maziwa, na vijito vyote vya Yuda vitatoa maji tele; na chemchemi itatokea katika nyumba ya BWANA, na kulinywesha bonde la Shitimu.