1. Kwa maana, angalieni, siku zile, na wakati ule, nitakapowarudisha mateka wa Yuda na Yerusalemu,
2. nitakusanya mataifa yote, nami nitawaleta chini katika bonde la Yehoshafau, na huko nitawahukumu kwa ajili ya watu wangu, na kwa ajili ya urithi wangu, Israeli, ambao wamewatawanya kati ya mataifa, na kuigawanya nchi yangu.
3. Nao wamewapigia kura watu wangu; na mtoto mwanamume wamemtoa ili kupata kahaba, na mtoto mwanamke wamemwuza ili kupata divai, wapate kunywa.
4. Naam, na ninyi ni kitu gani kwangu, enyi Tiro, na Sidoni, na nchi zote za Filisti? Je! Mtanirudishia malipo? Au mtanitenda neno lo lote? Upesi na kwa haraka nitawarudishia malipo yenu juu ya vichwa vyenu wenyewe.
5. Kwa kuwa mmetwaa fedha yangu na dhahabu yangu, nanyi mmevichukua vitu vyangu vyema vipendezavyo, na kuviingiza katika hekalu zenu;