22. Msiogope, enyi wanyama wa kondeni; maana malisho ya jangwani yanatoa miche, na huo mti unazaa matunda yake, mtini na mzabibu inatoa nguvu zake.
23. Furahini, basi, enyi wana wa Sayuni, mkamfurahie BWANA, Mungu wenu; kwa kuwa yeye huwapa ninyi mvua ya masika, kwa kipimo cha haki, naye huwanyeshea mvua, mvua ya masika, na mvua ya vuli, kama kwanza.
24. Na sakafu za kupepetea zitajaa ngano, na mashinikizo yatafurika kwa divai na mafuta.
25. Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu.
26. Nanyi mtakula chakula tele na kushiba, na kulihimidi jina la BWANA, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu; na watu wangu hawatatahayari kamwe.
27. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ni katikati ya Israeli, na ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, wala hakuna mwingine; na watu wangu hawatatahayari kamwe.
28. Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono;
29. tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.
30. Nami nitaonyesha mambo ya ajabu katika mbingu na katika dunia, damu, na moto, na minara ya moshi.
31. Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla haijaja hiyo siku ya BWANA iliyo kuu na itishayo.
32. Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayeliita jina la BWANA ataponywa; kwa kuwa katika mlima Sayuni na katika Yerusalemu watakuwako watu watakaookoka, kama BWANA alivyosema; na katika mabaki, hao awaitao BWANA.