26. Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu; lakini yeye aliyenipeleka ni kweli, nami niliyoyasikia kwake, ndiyo ninenayo katika ulimwengu.
27. Wala hawakutambua ya kuwa anawatajia Baba.
28. Basi Yesu akawaambia, Mtakapokuwa mmekwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo.
29. Naye aliyenipeleka yu pamoja nami, hakuniacha peke yangu; kwa sababu nafanya sikuzote yale yampendezayo.
30. Naye alipokuwa akisema hayo, wengi walimwamini.
31. Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli;
32. tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.
33. Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wo wote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru?