41. Basi Wayahudi wakamnung’unikia, kwa sababu alisema, Mimi ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni.
42. Wakasema, Je! Huyu siye Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa asemaje huyu, Nimeshuka kutoka mbinguni?
43. Basi Yesu akajibu, akawaambia, Msinung’unike ninyi kwa ninyi.
44. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho.
45. Imeandikwa katika manabii, Na wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu.
46. Si kwamba mtu amemwona Baba, ila yeye atokaye kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba.
47. Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna uzima wa milele.
48. Mimi ndimi chakula cha uzima.
49. Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa.
50. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife.
51. Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.