21. Basi wakataka kumpokea chomboni; na mara hiyo chombo kikaifikilia nchi waliyokuwa wakiiendea.
22. Siku ya pili yake mkutano waliosimama ng’ambo ya bahari waliona ya kuwa hakuna mashua nyingine huko ila moja, tena ya kuwa Yesu hakuingia katika mashua ile pamoja na wanafunzi wake, bali wanafunzi wake walikwenda peke yao.
23. (Walakini zikaja mashua nyingine kutoka Tiberia mpaka karibu na mahali pale walipokula mikate, wakati Bwana aliposhukuru.)
24. Basi mkutano, walipoona ya kuwa Yesu hayuko huko wala wanafunzi wake, waliingia mashuani wenyewe, wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu.
25. Hata walipomwona ng’ambo ya bahari, walimwambia, Rabi, wewe umekuja lini hapa?
26. Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.
27. Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu.
28. Basi wakamwambia, Tufanyeje ili tupate kuzitenda kazi za Mungu?
29. Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye.
30. Wakamwambia, Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani?
31. Baba zetu waliila mana jangwani kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale.
32. Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni.