12. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.
13. Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao.
14. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.
15. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu.
16. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.
17. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.
18. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni.
19. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli.