23. Naye Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu.
24. Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.
25. Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.
26. Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.
27. Sasa roho yangu imefadhaika; nami nisemeje? Baba, uniokoe katika saa hii? Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii.