Yn. 11:21-35 Swahili Union Version (SUV)

21. Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa.

22. Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa.

23. Yesu akamwambia, Ndugu yako atafufuka.

24. Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho.

25. Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;

26. naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?

27. Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni.

28. Naye alipokwisha kusema hayo, alikwenda zake; akamwita umbu lake Mariamu faraghani, akisema, Mwalimu yupo anakuita.

29. Naye aliposikia, aliondoka upesi, akamwendea.

30. Na Yesu alikuwa hajafika ndani ya kijiji; lakini alikuwa akalipo pale pale alipomlaki Martha.

31. Basi wale Wayahudi waliokuwapo na Mariamu nyumbani, wakimfariji, walipomwona jinsi alivyoondoka upesi na kutoka, walimfuata; huku wakidhania ya kuwa anakwenda kaburini ili alie huko.

32. Basi Mariamu alipofika pale alipokuwapo Yesu, na kumwona, alianguka miguuni pake, akamwambia, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa.

33. Basi Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliofuatana naye wanalia, aliugua rohoni, akafadhaika roho yake,

34. akasema, Mmemweka wapi? Wakamwambia, Bwana, njoo utazame.

35. Yesu akalia machozi.

Yn. 11