Yn. 10:18-29 Swahili Union Version (SUV)

18. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.

19. Kukaingia tena matengano kati ya Wayahudi, kwa ajili ya maneno hayo.

20. Wengi wao wakasema, Ana pepo huyu, tena ana wazimu; mbona mnamsikiliza?

21. Wengine wakasema, Maneno hayo siyo ya mtu mwenye pepo. Je! Pepo aweza kuwafumbua macho vipofu?

22. Basi huko Yerusalemu ilikuwa Sikukuu ya Kutabaruku; ni wakati wa baridi.

23. Naye Yesu alikuwa akitembea hekaluni, katika ukumbi wa Sulemani.

24. Basi Wayahudi walimzunguka, wakamwambia, Hata lini utatuhangaisha nafsi zetu? Kama wewe ndiwe Kristo, utuambie waziwazi.

25. Yesu akawajibu, Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia.

26. Lakini ninyi hamsadiki, kwa sababu hammo miongoni mwa kondoo wangu.

27. Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata.

28. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu.

29. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu.

Yn. 10