1. Laiti kichwa changu kingekuwa maji, na macho yangu kuwa chemchemi ya machozi, ili nipate kulia mchana na usiku kwa ajili yao waliouawa wa binti ya watu wangu!
2. Laiti ningekuwa na mahali pa kukaa jangwani, kibanda cha wasafiri; nipate kuwaacha watu wangu, na kuondoka kwao! Maana wao ni wazinzi, wote pia, mkutano wa watu wenye hiana.
3. Huupinda ulimi wao, kana kwamba ni upinde, ili kusema uongo; nao wamepata nguvu katika nchi, lakini si katika uaminifu; maana huendelea toka ubaya hata ubaya, wala hawanijui mimi, asema BWANA.
4. Jihadharini, kila mtu na jirani yake, wala msimtumaini ndugu awaye yote; maana kila ndugu atachongea, na kila jirani atakwenda huko na huko na kusingizia.
5. Nao watadanganya kila mtu jirani yake, wala hawatasema kweli; wameuzoeza ulimi wao kusema uongo; hujidhoofisha ili kutenda uovu.
6. Makao yako ya katikati ya hadaa; kwa hadaa wanakataa kunijua mimi, asema BWANA.
7. Basi, kwa hiyo BWANA wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawayeyusha na kuwajaribu; maana nisipotenda hivi, nitende nini kwa ajili ya binti ya watu wangu?
8. Ulimi wao ni mshale ufishao; husema maneno ya hadaa; mtu mmoja husema maneno ya amani na mwenzake kwa kinywa chake, lakini moyoni mwake humwotea.
9. Je! Nisiwapatilize kwa mambo hayo? Asema BWANA; na nafsi yangu je! Nisijilipize kisasi juu ya taifa la namna hii?