Yer. 8:11-22 Swahili Union Version (SUV)

11. Kwa maana wameiponya jeraha ya binti ya watu wangu kwa juu-juu tu, wakisema, Amani, Amani, wala hapana amani.

12. Je! Walitahayarika, walipokuwa wametenda machukizo? La! Hawakutahayarika, wala hawakuweza kuona haya usoni; basi wataanguka miongoni mwao waangukao; wakati wa kujiliwa kwao wataangushwa chini, asema BWANA.

13. Nitawaangamiza kabisa, asema BWANA; hapana zabibu katika mizabibu, wala tini katika mitini, hata jani lake litanyauka; na vitu vile nilivyowapa vitawapotea.

14. Mbona tunakaa kimya? Jikusanyeni, tukaingie ndani ya miji yenye maboma, tukanyamaze humo kwa maana BWANA, Mungu wetu, ametunyamazisha, naye ametupa maji yenye uchungu tunywe, kwa sababu tumemwasi BWANA.

15. Tulitazamia amani, lakini hayakuja mema yo yote; tulitazamia wakati wa kupona, na tazama, kufadhaika tu!

16. Kutoka Dani kumesikiwa mkoromo wa farasi zake; nchi yote pia inatetemeka kwa sauti ya mlio wa farasi zake za vita; maana wamekuja, wamekula nchi na vyote vilivyomo; huo mji na wote wakaao ndani yake.

17. Maana, tazama, nitatuma nyoka, naam, fira, kati yenu, wasioweza kutumbuizwa kwa uganga; nao watawauma, asema BWANA.

18. Laiti ningeweza kujifariji, nisione huzuni! Moyo wangu umezimia ndani yangu.

19. Tazama, sauti ya kilio cha binti ya watu wangu, itokayo katika nchi iliyo mbali sana; Je! BWANA hayumo katika Sayuni? Mfalme wake hayumo ndani yake? Mbona wamenikasirisha kwa sanamu zao walizochonga, na kwa ubatili wa kigeni?

20. Mavuno yamepita, wakati wa hari umekwisha, wala sisi hatukuokoka.

21. Kwa sababu ya maumivu ya binti ya watu wangu nimeumia mimi; nimevaa kaniki; ushangao umenishika.

22. Je! Hapana zeri katika Gileadi? Huko hakuna tabibu? Mbona, basi, haijarejea afya ya binti ya watu wangu?

Yer. 8