7. ndipo nitakapowakalisha mahali hapa, katika nchi hii niliyowapa baba zenu, tokea zamani hata milele.
8. Angalieni, mnatumainia maneno ya uongo, yasiyoweza kufaidia.
9. Je! Mtaiba, na kuua, na kuzini, na kuapa kwa uongo, na kumfukizia Baali uvumba, na kuifuata miungu mingine ambayo hamkuijua;
10. kisha mtakuja na kusimama mbele zangu katika nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, na kusema, Tumepona; ili mpate kufanya machukizo hayo yote?
11. Je! Nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, imekuwa pango la wanyang’anyi machoni penu? Angalieni, mimi, naam, mimi, nimeliona jambo hili, asema BWANA.
12. Lakini enendeni sasa hata mahali pangu palipokuwapo katika Shilo, nilipolikalisha jina langu hapo kwanza, mkaone nilivyopatenda kwa sababu ya uovu wa watu wangu Israeli.
13. Na sasa, kwa sababu mmezifanya kazi hizi zote asema BWANA, nami nikasema nanyi, nikiamka mapema na kunena, lakini hamkusikia; nami nikawaita wala hamkuniitikia;
14. basi, nitaitenda nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, mnayoitumainia, na mahali hapa nilipowapa ninyi na baba zenu, kama nilivyopatenda Shilo.
15. Nami nitawatupa ninyi mbali na macho yangu, kama nilivyowatupa ndugu zenu wote, yaani, wazao wote wa Efraimu.
16. Basi, wewe usiwaombee watu hawa, wala usiwapazie sauti yako, wala kuwaombea dua, wala usinisihi kwa ajili yao; kwa maana sitakusikiliza.