13. Na sasa, kwa sababu mmezifanya kazi hizi zote asema BWANA, nami nikasema nanyi, nikiamka mapema na kunena, lakini hamkusikia; nami nikawaita wala hamkuniitikia;
14. basi, nitaitenda nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, mnayoitumainia, na mahali hapa nilipowapa ninyi na baba zenu, kama nilivyopatenda Shilo.
15. Nami nitawatupa ninyi mbali na macho yangu, kama nilivyowatupa ndugu zenu wote, yaani, wazao wote wa Efraimu.
16. Basi, wewe usiwaombee watu hawa, wala usiwapazie sauti yako, wala kuwaombea dua, wala usinisihi kwa ajili yao; kwa maana sitakusikiliza.
17. Je! Huoni wanavyotenda katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu?
18. Watoto huokota kuni, na baba zao huwasha moto, na wanawake hukanda unga, ili kumfanyizia mikate malkia wa mbinguni, na kuwamiminia miungu mingine sadaka za kinywaji, wapate kunikasirisha mimi.
19. Je! Watu hawa wanikasirisha mimi? Asema BWANA; hawajikasirishi nafsi zao, na kuzitia haya nyuso zao wenyewe?
20. Kwa hiyo, Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, hasira yangu na ghadhabu yangu zitamwagwa juu ya mahali hapa, juu ya wanadamu, na juu ya wanyama, na juu ya miti ya mashamba, na juu ya mazao ya nchi; nayo itateketea, isizimike.
21. BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tieni sadaka zenu za kuteketezwa pamoja na dhabihu zenu, mkale nyama.
22. Maana sikusema na baba zenu, wala sikuwaamuru kwa habari za sadaka za kuteketezwa na dhabihu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri;
23. lakini naliwaamuru neno hili, nikisema, Sikilizeni sauti yangu, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru mpate kufanikiwa.
24. Lakini hawakusikiliza, wala kutega sikio lao, bali walikwenda kwa mashauri yao wenyewe, na kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, wakaenda nyuma wala si mbele.
25. Tokea siku ile baba zenu walipotoka katika nchi ya Misri hata leo, nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu ninyi, nikiamka mapema kila siku, na kuwatuma.