Yer. 6:18-30 Swahili Union Version (SUV)

18. Kwa sababu hiyo sikilizeni, enyi mataifa, mkajue, Ee kusanyiko, ni jambo gani litokealo kati yao.

19. Sikia, Ee nchi; tazama, nitaleta mabaya juu ya watu hawa, naam, matunda ya mawazo yao, kwa sababu hawakuyasikiliza maneno yangu; tena kwa habari ya sheria yangu, wameikataa.

20. Yafaa nini niletewe ubani kutoka Sheba, na uudi kutoka nchi iliyo mbali? Sadaka zenu za kuteketezwa hazikubaliwi, wala dhabihu zenu haziniridhii.

21. Basi, kwa hiyo, BWANA asema hivi, Tazama, nitaweka makwazo mbele ya watu hawa, na baba na wana wao watajikwaa pamoja; jirani ya mtu na rafiki yake watapotea.

22. BWANA asema hivi, Tazama, watu wanakuja, wakitoka katika nchi ya kaskazini; na taifa kubwa litaamshwa, litokalo katika pande za mwisho wa dunia.

23. Washika upinde na mkuki; ni wakatili, hawana huruma; sauti yao huvuma kama bahari, nao wamepanda farasi zao; kila mmoja kama mtu wa vita amejipanga juu yako, Ee binti Sayuni.

24. Tumesikia habari zake; mikono yetu inalegea; dhiki imetushika, na utungu kama wa mwanamke wakati wa kuzaa kwake.

25. Msitoke kwenda mashambani, wala msitembee njiani, kwa maana upanga wa adui uko huko; hofu ziko pande zote.

26. Ee binti wa watu wangu, ujivike nguo ya magunia, na kugaagaa katika majivu; fanya maombolezo, kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, maombolezo ya uchungu mwingi; maana mwenye kuteka nyara atakuja juu yetu ghafula.

27. Nimekuweka uwe mnara na ngome kati ya watu wangu; upate kuijua njia yao na kuijaribu.

28. Ni waasi kupita kiasi wote pia, waendao huko na huko wakisingizia, ni shaba na chuma hao, hutenda dhuluma wote pia.

29. Mifuo inafukuta kwa nguvu; risasi tu inatoka katika moto huo; mfua fedha ameyeyusha bure tu; maana wabaya hawaondolewi mbali.

30. Watu watawaita taka za fedha, kwa sababu BWANA amewakataa.

Yer. 6