Yer. 52:23-34 Swahili Union Version (SUV)

23. Palikuwa na makomamanga tisini na sita katika pande zake; makomamanga; yote yalikuwa mia juu ya wavu huo pande zote.

24. Naye amiri wa askari walinzi akamtwaa Seraya, kuhani mkuu, na Sefania, kuhani wa pili, na wale walinzi watatu wa mlango;

25. na katika mji akatwaa towashi mmoja aliyewasimamia watu wa vita; na watu saba katika wale waliouona uso wa mfalme, walioonekana katika mji; na karani wa jemadari wa jeshi, aliyewaandika watu wa nchi; na watu sitini katika watu wa nchi, walioonekana ndani ya mji.

26. Na Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawatwaa, akawaleta kwa mfalme wa Babeli huko Ribla.

27. Naye mfalme wa Babeli akawapiga na kuwaua huko Ribla katika nchi ya Hamathi. Ndivyo Yuda alivyochukuliwa utumwani, akatolewa katika nchi yake.

28. Watu hawa ndio wale ambao Nebukadreza aliwachukua mateka; katika mwaka wa saba, Wayahudi elfu tatu na ishirini na watatu;

29. katika mwaka wa kumi na nane wa Nebukadreza aliwachukua toka Yerusalemu watu mia nane na thelathini na wawili;

30. katika mwaka wa ishirini na tatu wa Nebukadreza, Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawachukua mateka katika Wayahudi watu mia saba na arobaini na watano; jumla ya watu hao wote ni watu elfu nne na mia sita.

31. Hata ikawa, katika mwaka wa thelathini na saba wa kuhamishwa kwake Yehoyakini, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa kumi na mbili, siku ya ishirini na tano ya mwezi, Evil-merodaki, mfalme wa Babeli, katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, akamwinua kichwa chake Yehoyakini, mfalme wa Yuda, akamtoa gerezani.

32. Akasema naye maneno mazuri, akaweka kiti chake juu ya viti vya wafalme waliokuwa pamoja naye huko Babeli.

33. Naye akabadili mavazi yake ya gerezani, akala chakula mbele yake daima, siku zote za maisha yake.

34. Na kwa posho yake, alipewa posho ya daima na mfalme wa Babeli; kila siku alipewa posho hata siku ya kufa kwake, siku zote za maisha yake.

Yer. 52