1. Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja hapo alipoanza kumiliki; naye akamiliki miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Hamutali, binti Yeremia wa Libna.
2. Naye alitenda yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na yote aliyoyatenda Yehoyakimu.
3. Maana, kwa sababu ya hasira ya BWANA, mambo haya yalitokea katika Yerusalemu na katika Yuda, hata akawaondosha wasiwe mbele za uso wake, naye Sedekia akamwasi mfalme wa Babeli.
4. Ikawa, katika mwaka wa kenda wa kumiliki kwake, katika mwezi wa kumi, na siku ya kumi ya mwezi huo, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akaja, yeye na jeshi lake lote, juu ya Yerusalemu, akapanga hema zake juu yake; nao wakajenga ngome juu yake pande zote.