Yer. 50:30-38 Swahili Union Version (SUV)

30. Kwa sababu hiyo vijana wake wataanguka katika njia kuu zake, na watu wake wa vita, wote pia, watanyamazishwa katika siku hiyo, asema BWANA.

31. Tazama, mimi ni juu yako, Ewe mwenye kiburi, asema Bwana, BWANA wa majeshi; maana siku yako imewadia, wakati nitakapokujilia.

32. Na mwenye kiburi atajikwaa, na kuanguka, wala hapana atakayemwinua; nami nitawasha moto katika miji yake, nao utawala wote wamzungukao pande zote.

33. BWANA wa majeshi asema hivi, Wana wa Israeli, na wana wa Yuda, wameonewa pamoja; na wote waliowachukua mateka wanawashika sana; wanakataa kuwaacha.

34. Mkombozi wao ni hodari; BWANA wa majeshi ndilo jina lake; yeye atawatetea kwa bidii, apate kuistarehesha nchi, na kuwasumbua wakaao katika Babeli.

35. Upanga u juu ya Wakaldayo, asema BWANA, na juu yao wakaao Babeli, na juu ya wakuu wake, na juu ya watu wake wenye hekima.

36. Upanga u juu ya hao wajisifuo, nao watapumbazika; upanga u juu ya mashujaa wake, nao watafadhaika.

37. Upanga u juu ya farasi zao, na juu ya magari yao ya vita; na juu ya watu wote waliochanganyika ndani yake, nao watakuwa kama wanawake; upanga u juu ya hazina zake, nazo zitaibwa.

38. Ukosefu wa mvua u juu ya maji yake, nayo yatakaushwa; maana ni nchi ya sanamu za kuchongwa, nao wameingiwa na wazimu kwa ajili ya sanamu.

Yer. 50