8. Walikuwa kama farasi walioshiba wakati wa asubuhi; kila mmoja akalia kwa kutamani mke wa mwenzake.
9. Je! Nisiwapatilize kwa sababu ya mambo hayo? Asema BWANA; na nafsi yangu, je! Nisijilipize kisasi juu ya taifa la namna hii?
10. Pandeni juu ya kuta zake mkaharibu, lakini msiharibu kabisa; ondoeni matawi yake; kwa maana si yake BWANA.
11. Maana nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda wamenitenda kwa hiana sana, asema BWANA.
12. Wamemkataa BWANA, na kusema, Si yeye; wala hayatatupata mabaya; wala hatutaona upanga wala njaa;
13. na manabii watakuwa upepo, wala neno lake halimo ndani yao; basi ndivyo watakavyotendwa.
14. Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala.
15. Angalia, nitaleta taifa juu yenu litokalo mbali sana, Ee nyumba ya Israeli, asema BWANA; ni taifa hodari, ni taifa la zamani sana, taifa ambalo hujui lugha yake, wala huyafahamu wasemayo.
16. Podo lao ni kaburi wazi, ni mashujaa wote pia.
17. Nao watakula mavuno yako, na mkate wako, ambao iliwapasa wana wako na binti zako kuula; watakula makundi yako ya kondoo na ya ng’ombe; watakula mizabibu yako na mitini yako; wataiharibu miji yako yenye boma, uliyokuwa ukiitumainia, naam, wataiharibu kwa upanga.
18. Lakini hata katika siku zile, asema BWANA, sitawakomesha ninyi kabisa.
19. Tena itakuwa mtakapouliza, BWANA ametutenda mambo hayo yote kwa sababu gani? Ndipo utakapowaambia, Vile vile kama ninyi mlivyoniacha mimi, na kuwatumikia miungu mingine katika nchi yenu wenyewe, ndivyo mtakavyowatumikia wageni katika nchi isiyo yenu.
20. Tangazeni neno hili katika nyumba ya Yakobo, litangazeni katika Yuda, kusema,
21. Sikilizeni neno hili, enyi watu wajinga msio na ufahamu; mlio na macho ila hamwoni; mlio na masikio ila hamsikii.
22. Je! Hamniogopi mimi? Asema BWANA; hamtatetemeka mbele za uso wangu; mimi niliyeweka mchanga kuwa mpaka wa bahari, kwa amri ya daima, isiweze kuupita? Mawimbi yake yajapoumuka-umuka, hayawezi kushinda nguvu; yajapovuma sana, hayawezi kuupita.
23. Lakini watu hawa wana moyo wa kuasi na ukaidi; wameasi, wamekwenda zao.
24. Wala hawasemi mioyoni mwao, Basi, na tumche BWANA, Mungu wetu, aletaye mvua, mvua ya mwaka, na mvua ya vuli, kwa wakati wake; na kutuwekea juma za mavuno zilizoamriwa.
25. Maovu yenu yameyageuza haya, na dhambi zenu zimewazuilia mema msiyapate.